ads

Saturday, March 24, 2018

Madai 6 ya Babu Seya yakwama Mahakama ya Afrika


MAHAKAMA ya Afrika ya Binadamu na Haki za Watu (ACHPR), imetupitilia mbali madai sita kati ya nane ya ukiukwaji wa haki za binadamu yaliyowasilishwa na mwanamuziki Nguza Viking (Babu Seya), na mwanawe, Johnson Nguza (Papii Kocha), katika mahakama hiyo.
Mwaka 2014, Nguza Viking na mwanaye Johnson walihukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwenda jela kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kunajisi na kulawiti watoto wadogo katika makazi yaliyopo Sinza jijini Dar es Salaam. Akisoma hukumu hiyo jana kwa niaba majaji saba waliokuwepo mahakamani hapo, Gerald Niyungeko kutoka nchini Burundi alisema ombi la kwanza la waombaji hao la kuachiwa huru haliwezi kutolewa kwa sababu limepitwa na wakatikufuatia Rais John Magufuli ameshawaachia.
Alisema madai ya pili ya kutopewa uhuru wa faragha ya kuwa na familia na kutoweza kujumuika kwenye jamii kufuatia kuwekwa mahabusu kinyume na haki za binadamu, mahakama hiyo imeona kuwa haina msingi na hivyo imetupilia mbali ombi hilo. Pia Jaji Niyungeko alisema mahakama hiyo imetupilia mbali maombi ya waombaji kuwa walikamatwa na polisi na kuwekwa mahabusu kwa muda wa siku nne bila kuonana na mwanasheria au mtu yoyote kwa kuwa huo ni utaratibu wa polisi kabla ya mtuhumiwa kufikishwa mahakamani.
Mahakama hiyo imetupilia mbali maombi ya Babu Seya na mwanawe kuwa walinyimwa haki ya kuwa na wakili wa kuwatetea na kudai kuwa ombi hilo siyo sahihi kwa kuwa kumbukumbu zilizopo zinaonesha waliwakilishwa katika mahakama za rufaa na wakili Mabere Marando. Aidha mahakama hiyo ilitupilia mbali madai kuwa ombi lao la waliokuwa wakitoa ushahidi dhidi ya kesi hiyo kufahamu makazi waliyokuwa wakiishi kwa kuwa walikuwa wakitembelea kila mara kutupiliwa mbali kwa kile mahakama ya Afrika ilichodai ushahidi wa hilo kutojitosheleza.
Madai mengine ambayo kwa mujibu wa Jaji Niyungeko yalitupiliwa mbali ni pamoja na maombi ya kwamba Nguza na mwanawe Johnson waliteswa ndani ya mahabusu na polisi kinyume na haki za binadamu, ambapo Mahakama ya Afrika ilidai kuwa ombi hilo pia halikuwa na ushahidi wa kutosha. Hata hivyo, kwa mujibu wa Jaji Niyungeko Mahakama hiyo ya Afrika ilikubaliana na madai ya waombaji hao kuwa Serikali ya Tanzania imekiuka haki zao kutokana na mahakama ya Tanzania kuwanyima fursa kupimwa kama Babu Seya alikuwa na uwezo wa kufanya tendo la ndoa.
Pia alisema mahakama hiyo baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, iligundua kuwa walalamikaji hawakupewa maelezo ya mashahidi na kuita mashahidi muhimu ili kuandaa utetezi wao vizuri. Kufuatia shauri hilo, mahakama imetoa siku 30 kwa waleta maombi kuwasilisha maombi ya fidia mahakamani hapo endapo wataamua kufanya hivyo kufuatia ukiukwaji wa haki zao na upande wa Serikali ya Tanzania nao utapewa kipindi kama hicho kujibu hoja za waleta maombi kabla ya mahakama kutoa maamuzi.
Nguza Viking na mwanawe hawakuwepo mahakamani hapo wakati hukumu hiyo ikisomwa na badala yake waliwakilishwa na wakili wao kutoka katika Taasisi ya Muungano wa Wanasheria Africa (PALU), Donald Dare. Akizungumzia hukumu hiyo, Wakili Dare alisema Mahakama ya Afrika imetoa maamuzi kulingana na ushahidi uliotolewa na kwamba kwa upande wake atawasiliana na mteja wake ili kujua kama wataamua kuwasilisha mahakamani hapo maombi ya fidia kutokana na vifungu vilivyokiukwa na Serikali ya Tanzania au la.

Nguza na mwanawe walifikisha maombi yao mbele ya mahakama hiyo mwaka 2015 katika kesi namba 006, wakidai kukiukwa kwa haki za binadamu katika kesi ya kunajisi na kulawiti iliyokuwa ikiwakabili na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela, kabla ya msamaha wa Rais, Desemba 9, mwaka jana.

No comments:

Post a Comment