BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), limesitisha udahili kwa muda kwa vyuo 163 kutokana na mapungufu mbalimbali ikiwemo miundombinu, walimu na vingine kufundisha programu ambazo hazijapitishwa na baraza hilo.
Aidha, baraza hilo limetoa orodha ya vyuo vilivyosajiliwa ambavyo vinaruhusiwa kupokea wanafunzi wapya kwa mwaka 2018 katika tovuti yake na kuwashauri waombaji wa udahili kwa msimu wa Machi/Aprili na udahili ujao, kuangalia iwapo chuo anachotaka kuomba kama kinaruhusiwa kudahili wanafunzi wapya. Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Nacte, Annastella Sigwejo alisema baraza hilo lina vyuo vingi ambavyo vimekidhi vigezo vya kupokea wanafunzi wapya kwa mwaka huu na vimewekwa katika tovuti ya Nacte.
“Tuna vyuo 459 ambavyo tulifanya ufuatiliaji na kukukuta baadhi vimefikia vigezo kwa kiasi fulani na tuliona vinaweza kuendelea ingawa vilikuwa na mapungufu madogo na vingine vina mapungufu makubwa na vyote tukavitaarifu na tukaviagiza vitupe taarifa kwamba vitawezaje kufikia ile hadhi inayotakiwa ili viweze kuruhusiwa kuendelea na udahili au kuendelea kutoa mafunzo” alisema Sigwejo.
Aliongeza, “Kuna baadhi vilijibu na kuleta taarifa kwamba vitafanya mabadiliko kwa muda fulani na tukavipa miezi mitatu na kuna vingine ambavyo havikuweza kabisa kuleta taarifa… ambavyo vimeleta taarifa tuliviruhusu viendelee kudahili wanafunzi na hivyo 163 ambavyo vimeshindwa kuleta taarifa.” Alisema kila chuo kilionekana na mapungufu yake, ambavyo baadhi vinatakiwa kutengeneza miundombinu itakayosaidia kufundisha, vingine vina upungufu wa walimu na vingine vina programu ambazo hazijapitishwa.
“Vyuo vyote vilitakiwa vijieleze na ambavyo havikuweza kufanya hivyo ndiyo tumevisitisha kwanza mpaka Baraza litakapokaa na kutoa maamuzi… Kwa sasa hatuwezi kusema kwamba vimefungiwa au havijafungiwa kwa kuwa baraza ndilo linatakiwa kutoa maamuzi hayo,” aliongeza mkurugenzi huyo. “Vyuo hivyo 163 havitaonekana kwenye tovuti na tumeshasema kwamba vyuo ambavyo havionekani kwenye tovuti haviruhusiwi kuchukua wanafunzi bali ni vile tu vilivyoonekana. Hivi bado vinafanyiwa tathmini kuona kama vitaweza kuendelea au havitaweza na maamuzi hayo yatatolewa kwenye kikao cha baraza ambacho kitakaa”.
Aidha, alisema vyuo ambavyo vimesajiliwa na Nacte ni 580 na vyuo ambavyo wamevipitia na kufanya tathmini ni vyuo 459 na kati ya hivyo, vyuo 296 ndivyo vimekidhi na vinaruhusiwa kudahili na kwamba ambavyo havijaruhusiwa kudahili ni vya fani tofauti. Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Udahili Nacte, Twaha Twaha alisema ili kumhakikisha mwanafunzi kwamba amedahiliwa kwenye chuo kinachotambuliwa na kozi anayosoma inatambuliwa, wameandaa mfumo unaoitwa ‘Students Information Verification System’ ambao utamuwezesha mwanafunzi kuhakiki taarifa zake.
“Mfumo huu unapatikana masaa 24 kwenye tovuti ya Nacte, hivyo mwanafunzi yeyote aliyepo chuoni au atakayekuwa amedahiliwa na chuo chochote, anaweza kuutumia mfumo huu kuangalia kama anatambuliwa na Nacte na kuangalia taarifa zake mbalimbali zinazowasilishwa na baraza,” alifafanua Twaha. Alisema katika udahili wa Machi/Aprili, 2018, Nacte ilitangaza udahili wa wanafunzi katika Astashahada na Shahada mbalimbali katika vyuo vyenye uwezo wa kupokea wanafunzi na udahili huo ulianza Februari 20, 2018 na utamalizika Machi 25, 2018, isipokuwa kozi ya afya ambayo mwisho wa udahili wake ni Aprili 10, mwaka huu.
Alisema baada ya udahili huo kufungwa, vyuo vyote vitatakiwa kuwakilisha Nacte majina ya wanafunzi waliochaguliwa kwa ajili ya uhakiki na kwamba chuo hakiruhusiwi kupokea mwanafunzi ambaye hawajamhakiki. “Nacte inakumbusha kwamba udahili wa muhula wa Machi/ Aprili 2018 hauhusishi programu zote za kada ya ualimu… kila mwaka tunaandaa na kutoa kitabu cha mwongozo wa udahili kinachoonesha vyuo, kozi zinazotolewa katika vyuo hivyo na sifa za kujiunga na kozi husika kinachopatikana katika tovuti yetu www.nacte.go.tz,” alisema bosi huyo wa Udahili. Hata hivyo, alisema katika kuhakikisha wanaendana na sera ya uchumi wa viwanda wamekuwa wakifanya ufuatiliaji kwenye vyuo vyao ili kuhakikisha elimu inayotolewa inakidhi viwango na kutengeneza mitaala inayomuandaa mtu kwenda kukidhi vigezo vya soko la ajira ili asiwe tegemezi na kujiajiri

No comments:
Post a Comment