ads

Friday, March 30, 2018

Utatu wa Samatta, Msuva, Kichuya wanoga Stars

ULE utatu wa washambuliaji watatu uliotengenezwa kwenye timu ya taifa, Taifa Stars baina ya Mbwana Samatta, Simon Msuva na Shizza Kichuya umeonekana kuzaa matunda kutokana na wanachokifanya wachezaji hao.
Hilo limedhihirika katika michezo miwili ya timu hiyo ya kirafiki ya kimataifa iliyopigwa hivi karibuni dhidi ya Algeria mjini Algiers na ule wa DR Congo uliochezwa Dar es Salaam juzi. Katika mechi ya Algeria licha ya kufungwa mabao 4-1 lakini utatu huo ulionekana kujipambanua kila wakati kuisumbua ngome ya ulinzi ya Algeria.
Stars katika mechi hiyo bao lake lilifungwa na Msuva akipokea kona safi iliyochongwa na Kichuya.
Pamoja na bao hilo lililopatikana kwa juhudi za wachezaji hao wawili lakini utatu huo ulionekana vizuri katika mechi ya Congo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo Stars ilishinda kwa mabao mawili na yote yalipatikana baada ya kugongeana vizuri kwa wachezaji hao watatu.
Bao la kwanza lilipatikana baada ya Msuva anayeichezea Difaa el Jadida ya Morocco kuumiliki vizuri mpira mbele ya mabeki watatu kabla ya kumpasia Kichuya pembezoni mwa uwanja ambaye alipiga krosi safi iliyotua kwa Samatta anayekipiga KRC Genk ya Ubelgiji aliyeunganisha wavuni mpira huo kwa kichwa.
Kama kawaida, bado la pili lilipatikana tena kwa Msuva kuukokota mpira kutoka katikati ya uwanja na kumpasia Samatta aliyemchungulia Kichuya na kumpa pasi nje ya 18 kabla ya winga huyo anayeichezea Simba kuachia shuti kali nje ya 18 lililomzidi maarifa kipa wa Congo, Ley Matampi na kutinga wavuni. Kutokana na ushindi huo, kocha msaidizi wa Stars, Hemed Morocco alisema kwa kifupi:

“Kiwango kizuri kilichooneshwa na wachezaji wetu, ukiangalia safu ya ushambuliaji ilipambana sana. Nidhamu ilikuwa kubwa zaidi ukilinganisha na mchezo uliopita na ndiyo imekuwa matunda ya kilichotokea.”

No comments:

Post a Comment