ads

Wednesday, March 28, 2018

90% ya uozo serikalini wasafishwa

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2016/17, imegusa mambo makubwa saba, ikiwemo udhibiti mkubwa na matumizi mazuri ya fedha za umma.
Kwa mujibu wa CAG, ofisi yake imetoa hati 561 ambapo hati 502 sawa na asilimia 90 zinaridhisha, hati 45 sawa na asilimia 8 zina mashaka, hati 7 sawa na asilimia 1 haziridhishi na hati 7 sawa na asilimia 1 ni mbaya.
Ripoti hiyo pia imebainisha kutolewa kwa hati chafu kwa baadhi ya halmashauri, utendaji mzuri wa Serikali Kuu na Deni la Taifa.
Maeneo mengine ni mamlaka za serikali za mitaa, utendaji wa mashirika ya umma, miradi ya maendeleo na ukaguzi maalumu.
Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Assad alimkabidhi Rais John Magufuli vitabu 6 vya ripoti hiyo, Ikulu, Dar es Salaam jana.
Ripoti hizo ni pamoja na ripoti ya Serikali Kuu, ripoti ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, ripoti ya Mashirika ya Umma, ripoti ya miradi ya maendeleo, ripoti ya Ukaguzi na Ufanisi na ripoti 10 zinazohusu ukaguzi wa ufanisi katika sekta mbalimbali.
Profesa Assad alisema serikali imeendelea kufanya vizuri, kwani kumekuwa na hatua nzuri ya kuongeza hati zinazoridhisha na kupunguza hati za mashaka na mbaya.
Alibainisha kuwa mashirika ya umma, yamepata hati safi kwa asilimia 96, Mamlaka ya Serikali za Mitaa asilimia 90 na Serikali Kuu imepata asilimia 86 kwa sababu ndani yake kuna vyama saba vya siasa ambavyo hakukuwa na makubaliano juu ya hesabu zake.
Baadhi ya vyama hivyo, kwa mujibu wa CAG, ni Tanzania Labour Party (TLP), Alliance for Tanzania Democratic Change, Demokrasia Makini na Chama cha Sauti ya Umma. Alisema sheria inamtaka kuvikagua vyama vyote vya siasa bila kujali kama vinapata ruzuku au la.
Serikali za Mitaa Baadhi ya halmashauri zilipata hati chafu. Halmashauri hizo ni Kigoma-Ujiji, Kigoma Vijijini na Pangani. Baada ya taarifa hiyo ya CAG, Rais Magufuli alimwagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo kuwasimamisha kazi wakurugenzi wa halmashauri hizo tatu kutokana na halmashauri zao kupata hati chafu.
Serikali Kuu Kwa mujibu wa Profesa Assad, kwa upande wa Serikali Kuu, kati ya taasisi 217 zilizokaguliwa, taasisi 204 zilipata hati safi ambayo ni sawa na asilimia 86; taasisi 22 ambazo ni sawa na asilimia tisa zimepata hati zenye shaka, wakati asilimia mbili ya taasisi hizo zikipata hati zisizoridhisha.
Aidha, katika eneo hilo pia, Prof Assad alisema kuwa kuna kesi za rufaa ya kodi zenye thamani ya Sh trilioni 4.4 ambazo mpaka sasa bado hazijafanyiwa uamuzi na Mahakama, wakati pingamizi za kodi zikigharimu Sh bilioni 739.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais Magufuli alimuagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kujadiliana na Jaji Mkuu ili kesi hizo ziamuliwe haraka.
Kwa mujibu wa CAG, walibaini kuwepo kwa mitambo ya kuchenjulia madini mkoani Mwanza, Shinyanga na wilayani Kahama kufanya kazi bila ya kuwa na leseni, hivyo kuingiza hasara ya Sh bilioni 232. Deni la Taifa Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, deni la Taifa limeongezeka kutoka Sh trilioni 41 mwaka uliopita hadi kufikia Sh trilioni 46 sasa.
Alisema kuwa kuna ongezeko la shilingi trilioni tano ambazo ni sawa na asilimia 12.
Mamlaka za serikali za mitaa Katika eneo hilo, CAG alisema kuwa Serikali za Mitaa 146 hazikupata Sh bilioni 582 kama sehemu ya bajeti ya maendeleo ya Serikali za Mitaa.
Aliongeza kuwa Sh bilioni 532 sawa na asilimia 51 ya fedha maendeleo, pia hazikupelekwa kweye serikali za mitaa 167. “Lakini pia fedha za miradi ya ndani kwenye Serikali za Mitaa hazikukusanywa aidha kwa kuwatumia mawakala au halmashauri zenyewe.
Serikali za Mitaa 140 hazikukusanya Sh bilioni 116 sawa na asilimia 22 ya mapato yake. Pia Profesa Assad alieleza kuwa vitabu 379 vya mapato hakuviona, hivyo hajui ni kiasi gani cha mapato kimepotea, lakini pia miradi mitatu yenye thamani ya Sh bilioni 1.6 kwenye Halmashauri za Biharamulo, Karagwe na Mpwapwa, imechelewa kukamilishwa.
Udhaifu mwingine alioubaini kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ni katika usimamizi wa rasilimali watu na udhibiti wa mishahara. Alisema kuwa kuna madai ya watumishi yanayofikia Sh bilioni 10.
Mashirika ya umma
Kwa upande wa mashirika ya umma, CAG alisema kuwa ofisi yake ilibaini udhaifu kwenye Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli nchini (RAHCO), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA).
Kwa upande wa NSSF, CAG alisema kuwa uliingia mkataba wa kutoa mkopo wa Sh bilioni 60, lakini akabaini kuwa malipo yaliyofanyika ni Sh bilioni 67, hivyo kulikuwa na ziada ya Sh bilioni 7, ambazo alisema huenda zimepotea.
Aidha, CAG alibaini kuwepo kwa usimamizi usiojitosheleza na usio madhubuti wa TPA kwenye kitengo cha makontena cha TICTS. Alisema kutokana na udhaifu huo, TPA inashindwa kupata kipato wanachostahili kutokana na kila kontena linaloingia hapo.
Miradi ya maendeleo Kwa mujibu wa Ripoti ya CAG, fedha za ushuru za mafuta na usafirishaji Sh bilioni 18 zilizokusanywa na TRA, hazikupelekwa kwenye Mfuko wa Barabara, lakini pia Mfuko wa Barabara nao haujalipa fidia ya Sh bilioni 12 kwa watu walioathiriwa na miradi maeneo mbalimbali nchini.

Aliongeza kuwa pia kumekuwa na ucheleweshaji wa malipo ya Sh bilioni 4 kwa wakandarasi. Ukaguzi maalumu Kwa mujibu wa CAG, baadhi ya taasisi kama vile Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kilikaguliwa na kubaini kuwa yalifanyika matumizi ya Sh milioni 3.5 bila kuidhinishwa na Katibu Mkuu na Mweka Hazina wa Chama hicho.

No comments:

Post a Comment