TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars jana iliwafuta machozi Watanzania kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi DR Congo katika mechi ya kimataifa ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Stars imepata ushindi huo ikiwa ni siku chache baada ya kupoteza kwa mabao 4-1 dhidi ya Algeria katika mechi nyingine ya kirafiki iliyochezwa mjini Algiers.
Mbwana Samatta na Shizza Kichuya ndiyo walikuwa nyota wa Stars jana, baada ya kufunga mabao hayo katika kipindi cha pili. Samatta aliifungia Stars bao la kuongoza katika dakika ya 74 kwa mpira wa kichwa akiunganisha krosi ya Kichuya ambaye alifunga bao la pili dakika ya 86, akipokea pasi ya Samatta.
Tangu mwanzo wa mchezo huo, timu hizo zilishambuliana kwa zamu huku washambuliaji wake wakitengeneza nafasi nyingi lakini walishindwa kuzitumia na kulazimika kwenda mapumziko kukiwa hakuna aliyeliona lango la mwenzake.
Congo walianza kipindi cha pili kwa mabadiliko ambapo waliwatoa Aaron Tshibola, Mubele Ndombe, Bennick Afobe na Yannick Bolasie na nafasi zao kuchukuliwa na Lema Mabidi, Junior Kabananga, Assombalanga Britt na Chadrac Akolo.
Mabadiliko hayo yaliibadilisha Congo na kufanya mashambulizi mfululizo langoni mwa Stars, lakini uimara na kujipanga vizuri kwa beki chini ya kipa Aishi Manula walijitahidi kuzuia hatari langoni mwao.
Hata hivyo, benchi la ufundi la Stars lilionekana kuendelea na ugonjwa uleule wa kufanya mabadiliko mpaka kelele kutoka kwa mashabiki zilipozidi.
Dakika ya 60 ndipo alipotolewa Mohamed Issa na nafasi yake kuingia Ibrahim Ajibu ambapo pia kidogo kulikuwa na mabadiliko.
Benchi la ufundi pia likiongozwa na Salum Mayanga lilifanya mabadiliko mengine dakika ya 75 kwa kumtoa Himid Mao na nafasi yake kuchukuliwa na Mudathir Yahya

No comments:
Post a Comment