ads

Saturday, March 24, 2018


GOLI alilojifunga beki wa kulia wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Shomari Kapombe katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Algeria limekuwa gumzo kila kona kila mmoja akiongea lake kuhusiana na kosa hilo na wengi wakimlaumu.
Hata hivyo, Kocha wa Singida United, Mdachi, Hans van Pluijm amemtetea mchezaji huyo akibainisha kuwa hakuna lawama yoyote juu yake na badala yake alifanya kazi ya ziada kutaka kuuokoa mpira, ambao mpaka unafika eneo lile lilikuwa kosa la mtu mwingine.
“Ndiyo amejifunga lakini halikuwa kosa lake na zaidi alitaka kuuokoa ule mpira, ukiangalia kwa makini, Kapombe alikuwa katikati ya washambuliaji wawili wakati inapigwa krosi na ilikuwa kosa la beki mmoja wa kati, ambaye hakufanya majukumu yake sawasawa.
“Kapombe alifanya kila liwezekanalo ili mpira ule usitue kwa adui, lakini bahati mbaya akajifunga, kimsingi halikuwa kosa lake na zaidi alipambana kuhakikisha ule mpira haufiki kwa adui aliyekuwa mbele yake,” alisema Pluijm kocha wa zamani wa Yanga.
Kapombe alijifunga bao hilo na kuiandikia Algeria bao la pili katika ushindi wa bao 4-1 walioupata juzi usiku katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Stade du 5 Juillet nchini Algeria.

Bao hilo lilipatikana baada ya Soffiane Hanni kuwachekecha mabeki wa Stars na kupiga krosi kwenye eneo la 18 lango la timu hiyo iliyowachonganisha mabeki wa Stars na washambuliaji wa Algeria, ambapo Kapombe alitokea nyuma kuja kujaribu kuuokoa mpira huo kabla ya kupiga kichwa na mpira kuzama wavuni.

No comments:

Post a Comment