ads

Saturday, March 24, 2018


SERIKALI ya Kuwait kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa nchi hiyo imeahidi kuipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 207.3 (sawa na Sh bilioni 466.4), kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mzunguko wa kuingia katikati ya mji wa Dodoma pamoja na mradi wa ujenzi wa barabara kutoka Morogoro hadi Dodoma yenye urefu wa kilometa 257.
Ahadi hiyo imetolewa mjini Dodoma na Balozi wa Kuwait nchini, Jassem Ibrahim Al-Najem, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.
Balozi Al-Najem amesema, mradi wa ujenzi wa barabara za mzunguko za kuingia na kutoka mjini Dodoma zitasaidia kuondoa msongamano wa magari yanayopita katikati ya mji huo kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na vyombo vya moto baada ya Makao Makuu ya Serikali kuhamia Dodoma.
Ameahidi kuwa nchi hiyo kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait na taasisi washirika (Mifuko ya Waarabu) wa mfuko huo, wataendelea kushirikiana na Tanzania kwa kutoa ufadhili wa ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo ya miundombinu na kilimo ili ikuze uchumi na maisha ya watu wake.
Katika kipindi cha miaka 40, Serikali ya Kuwait kupitia Kuwait Fund, imeipatia Tanzania mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 608 kwa ajili ya kutekeleza miradi 14 ya kiuchumi katika sekta za barabara, kilimo, umeme, maji na afya.

Dk Mpango ameishukuru Serikali ya Kuwait kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait kwa kuisaidia nchi kutimiza majukumu yake ya kuwaletea wananchi maendeleo kupitia mikopo yenye gharama nafuu inayotolewa na taasisi hiyo.

No comments:

Post a Comment